SALAMU ZA MKURUGENZI MKUU

DG

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

Kwa niaba ya watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ninawakaribisha nyote katika Tovuti hii ambayo ni uwanja rasmi wa kupata taarifa sahihi za jitihada na mafanikio ya Serikali katika kuzuia na kupambana na rushwa.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU ni chombo huru cha umma kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007. Kifungu cha 4 cha sheria hii, kikisomwa pamoja na kifungu cha 7 kinaeleza majukumu ya TAKUKURU ambayo yamegawanyika katika dhana kuu mbili ambazo ni Kuzuia Rushwa na Kupambana na Rushwa.

Katika kuzuia vitendo vya rushwa, TAKUKURU inafanya utafiti ili kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna ya kuondoa mianya iliyobainika. Vilevile, TAKUKURU inafuatilia matumizi ya rasilimali za umma zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili rasilimali hizo zitumike kwa kadri ya malengo yaliyokusudiwa, soma zaidi…

Vilevile, tunaelimisha umma juu ya rushwa na madhara yake kwa lengo la kuuhamasisha kushiriki katika mapambano hayo dhidi ya rushwa, soma zaidi…

Aidha, katika kupambana na vitendo vya rushwa nchini, Taasisi inachunguza tuhuma zote za makosa ya rushwa na kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka tunawafikisha mahakamani watuhumiwa wanaothibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa, soma zaidi…

Katika kutekeleza majukumu yetu hayo, Taasisi inazingatia Dira ya “Kuwa Taasisi Bora ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa” na Dhima ya “Kudhamiria Kuzuia na Kupambana na Rushwa” kwa kufanya kazi kwa misingi ya uadilifu, uwajibikaji na weledi.

Kwa msingi huo, natoa wito kwa wadau wa sekta zote kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuzuia na kupambana na rushwa nchini kwa kutekeleza kwa weledi, Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji. NACSAP I, NACSAP II, NACSAP III, na NACSAP IV.

Mkakati huu ni mwongozo wa Serikali unaotekelezwa kuanzia ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Kata hadi Kijiji na umeainisha ni kwa namna gani kila mmoja wetu anaweza kushirikiana na Serikali katika kuzuia na kupambana na Rushwa.

Kwa mara nyingine tena ninawakaribisha sana na ninawasihi msiache kufuatilia Tovuti yetu pamoja na mitandao mingine ya kijamii kwa anuani zetu zifuatazo:

Twitter: TAKUKURU.TZ               Instagram: takukuru.tz

Facebook: Takukuru Tz               You Tube: TAKUKURU TV

Ninawaomba Watanzania wote kila mmoja wetu kwa nafasi yake ashiriki mapambano dhidi ya rushwa kwakuwa KUPAMBANA NA RUSHWA NI JUKUMU LA KILA MMOJA WETU.

CP. SALUM R. HAMDUNI – MKURUGENZI MKUU