JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Na #####, Mara

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara imewahukumu wauguzi watatu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi 500,000 kwa makosa ya kughushi vyeti vya uuguzi na kujipatia ajira kinyume cha sheria. Wauguzi hao ni Lucy Wanjara, Elizabeth Nyirato na Asteria Nyirato.

 Baada ya kusoma hukumu hiyo Machi 30, 2017, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo  Mhe. Janeth Musarochi aliwapa washitakiwa nafasi ya kujitetea iwapo wana sababu za kuonewa huruma na Mahakama hiyo ili kupunguziwa adhabu kutokana na makosa waliyoyafanya.

 Akijitetea, mshitakiwa Lucy aliieleza Mahakama kwamba kwa sababu aliachishwa kazi hana uwezo wa kulipa kiwango chochote cha faini iwapo Mahakama itamuamuru hivyo. Kutokana na utetezi huo, Mahakama ilimhukumu kutumikia kifungo cha nje kwa kufanya kazi za jamii kwa kipindi cha miezi 12. Mhe. Musarochi aliiagiza ofisi ya Ustawi wa Jamii kumpangia mshtakiwa Lucy kituo cha kutekeleza adhabu hiyo. Washitakiwa Elizabeth na Asteria walilipa faini.

 Mwaka 2015, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mara ilipokea taarifa kuhusu washtakiwa hao kutumia vyeti vya kughushi na kujipatia ajira katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Uchunguzi ulibaini kuwa washtakiwa walighushi vyeti vya kidato cha nne na kuvitumia kuomba na kujipatia ajira ya uuguzi katika hospitali hiyo.

 Awali akisoma maelezo ya washtakiwa mahakamani hapo, mwanasheria wa TAKUKURU Bw. Marshal Mseja alisema kuwa kwa nyakati tofauti washtakiwa walitenda makosa hayo kinyume  cha kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007. Bw. Mseja alisema makosa hayo pia ni kinyume cha vifungu 333, 335(a), 337 na 342 vya Sheria ya Makosa ya Jinai namba 16 iliyoboreshwa mwaka 2002.