JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Na Juntwa Mwakujonga, Geita

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Geita, SACP Ladson Mwabulambo Mponjoli amewataka askari wa Jeshi la Polisi kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi ya Jeshi hilo na kutojihusisha na vitendo vya rushwa wanapotekeleza majukumu yao.  Wito huo aliutoa wakati wa semina iliyofanyika katika bwalo la Polisi Geita  Februari 23, 2017.

Akifungua semina hiyo, SACP Mponjoli  aliwaeleza washiriki hao kuwa wao ni  watumishi kama watumishi wengine wa umma na akawataka kuzingatia kanuni na mwongozo wa Jeshi la Polisi katika  kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu. Aliwaasa pia kudumisha nidhamu na utii kama ulivyo utamaduni wa Jeshi hilo.

Jeshi la Polisi ni mdau mmojawapo katika mapambano dhidi ya rushwa hivyo tuna wajibu wa kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa na kwa ushirikiano huo tutafanikiwa kulimaliza tatizo hili  nchini,” alisema Kamanda Mponjoli.

Mada kuu katika semina hiyo iliyowashirikisha askari 81 ilikuwa “Wajibu wa Askari wa Jeshi la Polisi katika Mapambano dhidi ya Rushwa.”   Semina hiyo ni utaratibu wa Jeshi hilo mkoani Geita kutoa mafunzo mbalimbali kwa askari polisi kila alhamisi ili kuwakumbusha wajibu wao katika kazi.

Akiwasilisha mada hiyo, Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Geita, Bw. Hajinas Onesphory alibainisha kuwa wananchi wanalilalamikia Jeshi hilo kwa mambo mengi ikiwemo kunyimwa fursa ya kuwadhamini ndugu zao wanapowekwa mahabusu. Alifafanua kwamba wananchi wanatoa mfano wa usemi “kuingia bure ila kutoka kwa pesa” kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za nchi na kinachorudisha nyuma vita dhidi ya rushwa.

Bw. Onesphory alisema malalamiko mengine yanahusu askari wa usalalama barabarani ambao wanatuhumiwa kuwashawishi wananchi wanaovunja Sheria ya Usalama Barabarani iliyoboreshwa mwaka 2002 kuwapatia rushwa ili wasichukuliwe hatua za kisheria. Wananchi hao pia wanalalamikia kitendo cha  kuombwa pesa ya mafuta ya gari la Polisi ili kwenda kushughulikia tukio la uhalifu au wanapohitaji msaada kutoka Jeshi hilo.

Akijibu baadhi ya malalamiko hayo, Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, ASP Julius Masanyiwa  alisema Jeshi la Polisi halina utaratibu wa kuwaomba watoa taarifa au waathirika wa matukio ya uhalifu pesa ya mafuta ya magari bali ni jukumu lao kuhakikisha wanapata mafuta ya kuwawezesha kufika kwenye matukio ya kihalifu. Alishauri kuwa mwananchi  akiombwa fedha ya mafuta na askari yeyote asisite kutoa taarifa ngazi za juu ili taratibu za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya askari huyo.

Naye Bw. Juntwa Mwakujonga aliyeambatana na Bw. Onesphory, aliwakumbusha washiriki kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria wakiwemo Askari Polisi na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya rushwa anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Bw. Mwakujonga pia aliwaasa askari hao kutosheka na vipato vyao kwani baadhi ya watumishi huwa hawaridhiki na vipato hivyo na kutaka kuongezewa mshahara. Aliwaambia kuwa mshahara mdogo kisiwe kisingizio cha kujihusisha na vitendo vya rushwa.

TAKUKURU Geita yaonyesha njia: yaitaka jamii ilinde haki za wenye ulemavu na kuwashirikisha katika mapambano dhidi rushwa

Na Barnabas Mushi, Bukombe

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inaitaka jamii itambue kwamba pamoja na kuwa rushwa ni adui wa haki lakini kumficha mtoto au mtu mwenye ulemavu ni kumnyima haki za msingi za kibinadamu. Jamii ielewe pia kwamba suala la elimu na fursa kwa watu wenye ulemavu sio jambo la hiari bali la lazima na ni moja kati ya haki za binadamu.

Hivyo, wakati tunapambana na rushwa ili isitunyang’anye haki, haina budi pia kila mwanajamii akahakikisha kila mtu mwenye ulemavu anapata haki anazostahili kama vile malezi, afya, elimu na makazi bora ili awe mwanajamii muadilifu na mwenye mchango chanya kwa maendeleo ya Taifa. Hatua hii inapaswa pia kuendana na kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa sababu wao ni sehemu ya jamii inayoathirika na vitendo vya rushwa.

Mtizamo huu ni kati ya mambo yaliyowafanya watumishi wa ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Geita na wilaya za Chato na Bukombe kuwatembelea na kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa kusikia, kuongea na mtindio wa ubongo wanaolelewa katika kituo cha Shule ya Msingi Ushirombo, wilayani Bukombe. Ziara hiyo ya TAKUKURU ya Januari 17, 2017 pia ililenga kuwaelimisha watendaji wa shule hiyo kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na kukuza ushirikiano kati ya Taasisi na jamii hiyo inayoihudumia. Msaada huo wa tani moja ya mifuko ya saruji ulilenga kusaidia ujenzi wa uzio wa kituo ambao ulikuwa changamoto kubwa katika kuimarisha ulinzi wa watoto hao.

Akiongea wakati wa tukio hilo fupi, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Geita, Bw. Musa Chaulo alisema Taasisi inatambua kuwa mapambano dhidi ya rushwa yatafanikiwe kwa kushirikiana  na jamii nzima. Alieleza kwamba TAKUKURU inashirikiana na jamii kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, kuhamasisha maendeleo na kutoa michango mbalimbali ili kujenga ustawi wa jamii na kuhamasisha utawala bora.

Aidha, aliupongeza uongozi na walimu wa kituo hicho kwa kuwalea watoto hao na kuwaomba wasikate tamaa kutokana na changamoto wanazokumbana nazo bali waendelee kufanya kazi  kwa upendo wakitarajia zaidi baraka kutoka kwa Mungu.

Mkuu wa kituo hicho, Bw. ##### alieleza kuwa kituo kilianza mwaka 2009 kikiwa na mwalimu mmoja na wanafunzi saba na hakikuwa na jengo ambapo watoto walisomea chini ya miti. Mwaka 2012 Halmashauri ya wilaya ya Bukombe ilijenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu na kutoa meza 25, viti 25 na makabati matatu.

Alieleza kuwa Serikali Kuu nayo ilianza kutoa ruzuku kwa ajili ya chakula cha watoto na wizara ikaongeza walimu. Mpaka Desemba 2016, kituo kilikuwa na walimu watano na wanafunzi 40. Watoto wenye ulemavu waliopo kituoni ni wenye mtindio wa ubongo na ububu. Bw. ### aliishukuru Serikali kwa jitihada hizo hata hivyo alisema kituo bado kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo upungufu wa vifaa na mwamko mdogo wa jamii kuunga mkono shughuli zinazofanywa na kituo.

Mkuu wa TAKUKURU Bukombe Bw. Chuzela Shija  aliushukuru uongozi wa kituo kwa kukubali kupokea ziara ya watumishi wa TAKUKURU na kuwasihi waendelee kushirikiana na Taasisi katika vita dhidi ya rushwa. Alisema hatua hiyo pamoja na manufaa mengine, itaongeza tija katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Bukombe na akawaasa watumishi wa Halmashauri kutekeleza miradi hiyo kwa kuzingatia thamani ya fedha. Bw. Shija aliwatahadharisha kuwa TAKUKURU itawachukulia hatua za kisheria watumishi wote watakaobainika kufanya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.

Mkuu wa TAKUKURU Chato Bw. Zabroni Sabai aliwashukuru na kuwapongeza walimu na uongozi wa kituo  kwa kazi nzuri wanayoifanya. Alishauri elimu zaidi itolewe kwa wazazi wengine wenye watoto kama hao waliofichwa majumbani ili wajiunge katika kituo hicho na kupata msaada na malezi yatakayowasaidia katika maisha yao. “Familia zenye watu wenye ulemavu zinatambua kwa dhati uzito wa jukumu hili hivyo kazi mnayoifanya ni takatifu sana na ni sadaka njema katika maisha yenu na familia zenu”, alisema Bw. Sabai.

Diwani wa kata ya Bulangwa, Bw.Yusuph Mohamed aliishukuru TAKUKURU kwa msaada huo na kueleza kuwa Halmashauri ya Bukombe imeomba shilingi milioni 36 na zipo kwenye hatua nzuri ya kutolewa na Serikali kwa ajili ya kutatua changamoto za kituo hicho.

 

 

 

 

­­