JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Ofisa forodha msaidizi TRA Kizimbani kwa kujilimbikizia mali

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) imemfikisha  mahakamani ofisa forodha msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye kituo chake cha kazi ni Mapato House, Jenifer Emanuel Mushi, kwa makosa mawili ya rushwa.

Mshtakiwa alipandishwa kizimbani Oktoba 24, 2017 na kusomewa mashtaka na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Vitalis Peter, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kati ya Machi 21, 2016 na Juni 30, 2016 mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa umma alitenda kosa la kupatikana akimiliki magari 18 yenye thamani ya Shilingi 197,601, 207/= ambayo hailingani na mapato yake halali kinyume na kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia Rushwa na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Kosa la pili linalomkabili ni kuwa kati ya Machi 21, 2012 na Machi 30, 2016 akiwa mwajiriwa wa umma aliishi kiwango cha maisha kinachofikia Shilingi 333,255,556.24 ambacho hakilingani na mapato yake halali kinyume na kifungu cha 27(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia Rushwa na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007. 

Mshtakiwa alikana mashtaka dhidi yake na upande wa mashtaka uliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ambayo ingeona inafaa kwa ajili ya usikilizaji wa hoja za awali kwa kuwa uchunguzi wa shaauri umekamilika.

Mshtakiwa kupitia kwa wakili wake wa kujitegemea, Elisalia Mosha, aliiomba mahakama kumpaitia dhamana kwa sababu mashtaka dhidi yake yanadhaminika kisheria.

Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo yalikuwa ni kuwa na mdhamini mmoja ambaye alitakiwa kusaini bondi ya Shilingi milioni 20 na kesi imeahirishwa hadi Novemba 7 mwaka huu itakapokuja kwa usikilizaji wa hoja za awali.