JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Historia ya Taasisi

Historia ya Taasisi na jitihada za kupambana na rushwa nchini

Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (TAKUKURU) ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007. Sheria hii ilitungwa baada ya kufutwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) Sura ya 329 iliyofanyiwa marrejeo mwaka 2002. Kuanzishwa kwa chombo hiki kulikuja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Mswaada wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2007 mnamo tarehe 16 Aprili, 2007. Mswaada huu ulisainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Kikwete kuwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mnamo tarehe 11Juni, 2007 na ilianza kufanya kazi tarehe 1Julai, 2007.

Mapambano dhidi ya rushwa nchini yalianza hata kabla ya Uhuru. Baada ya uhuru Tanzania ilirithi sheria ya kikoloni ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1958 iliyokuwa na chimbuko lake tangu mwaka 1930. Mwaka 1930 utawala wa Kiingereza ulitumia Kanuni ya Adhabu ya India (The Indian Penal Code) kuwaadhibu watumishi wa Serikali ya kikoloni waliopatikana na hatia ya kuomba na kupokea hongo. Sheria hii ilikuwa na vipengele vichache sana dhidi ya rushwa kama vile kuomba na kupokea hongo. Vipengele vya sheria hii juu ya rushwa viliingizwa kwenye sheria ya makosa ya Jinai, Sura ya 16 iliyotungwa na Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika lililojulikana kama LEGICO (Legislative Council) mnamo mwaka 1945. Hii ilikuwa Sheria ya kwanza ya Kanuni za Adhabu Tanganyika iliyoanza kutumika kudhibiti vitendo vya hongo na matumizi ya nyaraka zenye taarifa za uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri. Mwaka 1958 LEGICO ilitunga Sheria ya Kuzuia Rushwa (Sura ya 400) ambayo pia ilirejea vipengele vilivyokuwa katika Sheria ya Makosa ya Jinai na ililenga kudhibiti vitendo vya rushwa kwa watumishi wa umma. Kimsingi kutungwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sura ya 400, kulitokana na ukweli kwamba Sheria ya Makosa ya Jinai , Sura ya 16, ilikuwa imeshindwa kuzuia au kupambana na rushwa ipasavyo.

Baada ya uhuru utumishi wa umma ulipanuka kwa kasi.Watumishi walianza kwenda kinyume na maadili ya kazi na walianza kutumia nafasi zao kama vitega uchumi. Mnamo mwaka 1970 Sheria ya Kuzuia Rushwa (Sura ya 400) ilifanyiwa marekebisho na kuongeza kosa la mtumishi wa umma kupatikana na mali zilizopatikana kwa njia za rushwa. Hata hivyo mnamo mwaka 1971 sheria hii ilifutwa na kutungwa Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sheria namba 16 ya mwaka 1971 (Sura ya 329) baada ya kuonekana kushindwa kupambana na rushwa katika mazingira ya wakati huo. Sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971 ilinakili vipengele vyote vya Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sura ya 400 na kuongeza makosa mengine kadhaa.

 Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi iliyolikabili Taifa Sheria ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1971 haikuweza kupunguza kasi ya rushwa nchini. Kuadimika kwa bidhaa muhimu, magendo, na ulanguzi vilichochea kasi ya ueneaji wa rushwa nchini. Rushwa ilianza kuingia katika vyombo vya dola jambo ambalo lililazimu serikali Mnamo mwaka 1974 kuifanyia marekebisho sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971 kupitia Sheria Namba 2 ya mwaka huo, kwa lengo la kuanzishwa kwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa (The Anti – Corruption Squad – ACS) ambacho kilianza kufanya kazi mnamo tarehe 15Januari, 1975 kwa tamko la serikali Namba 17 la mwaka 1975. Kabla ya kikosi hiki kuanzishwa shughuli za kuzuia rushwa zilifanywa na Jeshi la Polisi. Kikosi cha Kuzuia Rushwa kilikuwa na kazi kuu tatu, yaani kuzuia rushwa, kupeleleza na kuendesha mashtaka dhidi ya watuhumiwa wa makosa ya rushwa nchini. Kikosi hiki kilikuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na kilikuwa na mamlaka ya kupambana na wala rushwa katika utumishi wa Umma au mashirika yake na viongozi wa serikali. Hivyo kikosi hakikujihusisha na rushwa katika sekta binafsi nchini.

Wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili hususani miaka ya 1980 mwishoni Serikali iliboresha masharti ya biashara kwa kuruhusu uchumi wa soko huria na kufanya sekta binafsi kukua kwa kasi.Vilevile katika kipindi cha awamu ya pili ya uongozi wa nchi serikali iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwanzonini mwa mwaka 1990. Ili kukidhi mabadiliko hayo ya kiuchumi na kisiasa Sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya Mwaka 1971 (Sura ya 329) ilifanyiwa marekebisho mengine mwaka 1991. Katika marekebisho hayo ya kisheria Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) ilianzishwa rasmi kuchukua nafasi ya Kikosi cha Kupambana na Rushwa kwa tamko la Serikali Na.27 la mwaka 1991. Mabadiliko yalilenga kukifanya chombo hicho kifanye kazi zake kwa mbinu za kisayansi na uhuru zaidi. Wakati huo Taasisi ilikuwa na Idara tatu ambazo ni Idara ya Utawala na Utumishi, Idara ya Sheria na Mashtaka na Idara ya Mafunzo, Utafiti na Elimu kwa Umma.

Kutungwa kwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya 2007

Kutokana na maendeleo ya sayansi, teknolojia, utandawazi, mabadiliko ya uchumi na kisiasa katika miaka ya 1980 na mwanzoni mwa mwaka 1990 , yaliyotokea nchini na duniani kote pamoja na kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya rushwa, Sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971 ilianza kuonekana kushindwa kuzuia na kupambana na rushwa. Baada ya kung’amua hilo, serikali iliamua kuanzisha jitihada za kuangalia namna ya kuiboresha sheria hii ikiwa ni pamoja na:

 • Tume ya Rais ya kuchunguza kero za rushwa nchini maarufu kama tume ya Warioba iliyoteuliwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa, tarehe 17 Januari, 1996.

 • Kamati ya wataalamu kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Taasissi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) kwa ajili ya kuangalia namna ya kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Warioba mwaka 2000.

 • Kamati ya wataalamu kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi, Kitivo cha Sheria ( Chuo Kikuu cha Dar es salaam ) na TAKURU mnamo mwaka 2003.

 • Ripoti ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ya mwaka 2004; na

 • Kamati maalumu ya wataalamu kutoka TAKURU, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Idara ya Mahakama, Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu, Ikulu na Benki Kuu ya Tanzania mnamo mwaka 2005.

Kimsingi, makundi yote haya ya watalaam yaligundua kuwa kulikuwa na mapungufu makubwa kwa upande wa TAKURU katika vita dhidi ya rushwa nchini ikiwa ni pamoja na :

 • Kutokuwepo uhakika wa ajira ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKURU;

 • Kazi za TAKURU kutoainishwa vizuri;

 • Baadhi ya makosa ya rushwa kutofanywa ya jinai;

 • TAKURU kutowasilisha taarifa zake Bungeni;

 • Kutokuwepo vipengele katika Sheria ya Kuzuia Rushwa ya Mwaka 1971 vinavyowalinda maofisa wa TAKURU dhidi la tishio la kushtakiwa kutokana na shughuli zao;

 • Kutokuwepo vipengele vinavyozuia rushwa katika manunuzi na mikataba ya Serikali na kandarasi za Serikali; na

 • Kutokuwepo vipengele vya kisheria vinavyozuia rushwa katika sekta binafsi.

Hivyo, ili kuifanya vita dhidi ya rushwa iwe na mafanikio, ilipendekezwa kwamba wakati ulikuwa umefika wa kuifuta Sheria ya Kuzuia Rushwa ya Mwaka 1971 na kutunga nyingine yenye meno madubuti ya kuzuia na kupambana na rushwa. Kwa sababu hizi serikali ilipeleka muswaada wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwezi Februari, 2007. Kupitia mswaada huu Sheria ya Kuzuia Rushwa Na.16/1971 ilifutwa na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007 ilipitishwa na Bunge mwezi Februali 2007 na ilianza kutumika rasmi tarehe 01 Julai 2007. Kufuatia kutungwa kwa Sheria hii, jina la Taasisi ya Kuzuia Rushwa lilibadilishwa na kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Shabaha ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007

Kwa mujibu wa Utangulizi wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007, Sheria hii imetungwa kwa shabaha ya kuanzisha na kuipa nguvu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili iweze kushughulikia kikamilifu makosa ya rushwa na yale yanayofanana nayo hapa nchini. Sheria hii inatumika Tanzania Bara peke yake na inahusu kila mtu atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa awapo nchini Tanzania au anapokuwa nje ya Tanzania au alikuwa nje ya Tanzania na kwa wakati huo anaishi Tanzania .

Madhumuni ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007

Lengo kuu la Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007 limeainishwa katika kifungu cha 4 cha Sheria hii ikiwa ni kuhakikisha ustawi wa utawala bora na kuondoa rushwa nchini. Ili kuhakikisha lengo hili linatimia, sheria hii inaweka mazingira bora kisheria, kiutawala, na kiutekelezaji yenye mwelekeo wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini. Hivyo, sheria hii itawezesha:

 • Kuwepo ushauri juu ya mienendo na taratibu mbalimbali katika utekelelezaji wa shughuli za umma, mashirika ya umma, taasisi binafsi nchini kwa lengo la kuifanyia kazi ya kung’amua na kuzuia rushwa kuwa ya ufanisi

 • Upatikanaji wa habari au taarifa mbalimbali kuhusu athari za rushwa na vitendo mbalimbali vya rushwa nchini;

 • Kuwezesha au kufanikisha ushirikiano mzuri na wenye manufaa kati ya taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, zinazojihusisha na mapambanodhidi ya rushwa ;

 • Kuhimiza ustawi, na kuimarisha ushiriki wa umma kwa ujumla katika kupambana na rushwa nchini ,na

 • Kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi, upelelezi na uendeshaji wa mashtaka dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa nchini.

UONGOZI WA TAKUKURU

Kati ya mwaka 1973 – 1990 Taasisi (TAKURU)  iliongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakurugenzi Wasaidizi chini ya Idara zao. Kati ya  mwaka 1991- 2007 Taasisi iliongozwa na Mkurugenzi Mkuu akisaidiwa na Wakurugenzi wa Idara. Kuanzia mwaka 2007 hadi sasa TAKUKURU imekuiwa ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu akisaidiwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu na Wakurugenzi wa Idara na huteuliwa na Rais. Toka mwaka 1973 hadi sasa TAKUKURU imeongozwa na Wakurugenzi wafuatao :

 • 1973 – 1974: Ndugu Geofrey Sawaya

 • Machi,1974 – Juni,1975: Ndugu S. Rutayangirwa

 • Juni,1975 -1990: Ndugu Zakaria Maftah

 • April,1990 – Novemba, 2006: Major General (Rtd), Anatory Ruta Kamazima

 • Novemba, 2006 – Disemba, 2015: Dr. Edward Gamaya Hoseah

 • Machi, 2015 - Septemba 2018: Ndugu Valentino Longino Mlowola

 • Septemba, 2018 - Hadi Sasa: Kamishina wa Polisi Diwani Athumani Msuya