JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

Harbinder Sing Sethi na James Rugemarila Wapandishwa Kizimbani

Na Mussa Misalaba

Watuhumiwa wawili wa sakata la uchotaji wa mabilioni ya fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow wamepandishwa kizimbani Juni 19, 2017 wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi na kuisababishia hasara Serikali mabilioni ya fedha.

Waliofikishwa mahakamani ni Mwenyekiti Mtendaji wa Power African Power Solution Ltd, Harbinder Singh (59) na Mkurugenzi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing James Buchard Rugemarila (71).

Washtakiwa walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, Huruma Shaidi, na kusomewa mashtaka ambayo hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi na kutoa maamuzi ya dhamana.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akisaidiana na Wakili wa Serikali Paul Kadushi  aliyesoma mashtaka, na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Joseph Kiula.

 Katika shtaka la kwanza Kadushi aliiambia Mahakama kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika sehemu tofauti za Dar es Salaam,Tanzania, Kenya, Afrika  Kusini na India  washtakiwa kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka  la pili upande wa Mashtaka uliiambia Mahakama kuwa  kati  ya  Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 Jijini  Dar es Salaam washtakiwa kwa pamoja na wakiwa siyo watumishi wa Umma lakini kwa kushirikiana na Watumishi wa Umma walijihusisha na mtandao wa uharifu wa jinai kwa lengo la kujipatia faida au manufaa mengine.

Katika shtaka la tatu  Kadushi alidai kuwa Oktoba 18, 2011 Sethi akiwa mtaa wa Ohio, Ilala, Dar es Salaam  na akiwa na nia ovu alighushi fomu namba 14a ya Usajili wa  Kampuni na  kuonyesha  kuwa yeye ni Mtanzania aishiye kwenye Kitalu namba 887, Mtaa wa Mrikau, eneo la Masaki,  Dar es Salaam wakati siyo kweli

Katika shtaka la nne Kadushi alidai kuwa Oktoba18, 2011 Sethi alitoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14a ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera, ikionyesha kuwa yeye ni Mtanzania na anaishi Kitalu namba 887, Mtaa wa Mrikau, eneo la Masaki, Dar es Salaam wakati siyo kweli.

Aidha, Kadushi alidai katika shtaka la tano kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014

washtakiwa wakiwa na hila na nia ya kufanya ulaghai wakiwa maeneo ya  Benki ya Stanbic, tawi la Kati, wilaya ya Kinondoni na Benki ya Mkombozi, tawi la Mtakatifu  Joseph wilaya ya Ilala, Dares Salaam walijipatia toka Benki Kuu ya Tanzania  fedha za Kimarekani  Dola 22,198,544.60 na fedha za Kitanzania Sh.309,461,300,158.27.

Pia,washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya fedha za Kimarekani Dola 22,198,544.60 na fedha za Kitanzania Sh.309,461,300,158.27 walizozikwapua toka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kupitia Benki ya Stanbic,tawi la Kati, Kinondoni (USD 22,198,544.60) na  Benki ya Mkombozi, tawi la Mtakatifu  Joseph,  Ilala, Dares Salaam(Tshs309,461,300,158.27) kati ya  Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014.

Baada ya washtakiwa kusomewa  mashtaka na Wakili wa Serikali Paul Kadushi, Wakili wa Serikali Mkuu, Faranja Nchimbi aliiambia Mahakama kuwa uchunguzi wa kesi bado unaendelea na aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Upande wa utetezi uliokuwa na mawakili wanne ambao ni Michael Ngalo, Respicius Didace,Carthbert Tenga na Onesmo Mpenzile uliiomba mahakama iwapatie wateja wake dhamana kwa masharti itakayoona yanafaa kwa sababu mashtaka dhidi yao yanadhaminika.

Hata hivyo, upande wa mashtaka uliiomba Mahakama kuyatupilia mbali maombi ya upande wa utetezi ya kuwapatia dhamana washtakiwa kwa kuwa haina mamlaka ya kutoa dhamana wala kusikiliza maombi ya dhamana yao na kuongeza kuwa ndiyo maana washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote waliposomewa mashtaka.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 12, kifungu kidogo cha (4) cha sheria ya uhujumu uchumi, DPP hajawasilisha kibali cha kuruhusu mahakama hii kusikiliza kesi hii na pia kifungu cha 29, kifungu kidogo cha (4) aya (d) cha sheria hiyo kinatafsiri kuwa thamani ya fedha ikizidi million kumi dhamana yake inasikilizwa na mahakama kuu”, alidai Kadushi.

Hakimu Shaidi alisema Mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza na kutolea maamuzi ya kesi hiyo hadi DPP atakapowasilisha kibali na alisema kwa kuwa upelelezi haujakamilika kesi hiyo itatajwa Julai3, mwaka huu na akaamuru washtakiwa waende mahabusu. “Mlango uliowazi ni mawakili wa washtakiwa kwenda mahakama kuu Tanzania, kanda ya Dar es Salaam, kuomba dhamana”, alisema hakimu.

Sakata la mazingira tata ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha toka akaunti ya Tegeta Escrow iliyopo Benki Kuu ya Tanzania liliibukia Bungeni mwaka 2014 na kuwa gumzo kila kona ambapo Bunge la Jamhuri lilipitisha maazimio manane  na mojawapo likiwa ni kufanyika kwa uchunguzi na kukamatwa wote waliohusika na kashifa hii.

Sakata la Escrow lilihusisha uchotwaji  wa mabilioni ya fedha toka akaunti  ya Tegeta Escrow iliyopo Benki kuu ya Tanzania (BOT), iliyofunguliwa kwa pamoja na TANESCO na IPTL ili kusubiri kumalizika kwa mgogoro kati ya taasisi hizi juu ya tozo za ufuaji umeme (capacity charges).

Kufuatia tatizo la umeme nchini mwaka 1994, Serikali iliingia mkataba na IPTL wa kuuziwa umeme unaozalishwa kwa njia ya machine za diesel katika eneo la Tegeta, Dar es Salaam na ilikuwa ikimilikiwa na Mechmar ya Malasia (70%) na VIP Engineering and Marketing Limited(30%).