Mahakama ya Wilaya ya Makete imefungua kesi ya Uhujumu Uchumi Namba 8510/2025 mbele ya Mhe. Msacky Ivarn, Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Wilaya ya Makete dhidi ya Mwenyekiti Mstaafu wa Kijiji cha Mago Bw. ATHANAS MGIMBA CHAULA pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Mago Bw. ALLY JAILOSI SANGA.
Washtakiwa wameshtakiwa kwa makosa mawili ya Ubadhirifu kinyume cha kifungu cha 28(1) na Matumizi Mabaya ya Mamlaka kinyume cha kifungu cha 31, vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 R.E 2022.
Akisoma hati ya mashtaka Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Yahaya Mkongwa amesema washtakiwa hao wawili walichaguliwa katika Kamati ya Utatuzi wa mgogoro wa ardhi na mipaka kati ya Kijiji cha Mago na Kijiji cha Ibaga, ambapo walijikusanyia fedha ya kodi ya ardhi kwa wananchi waliokuwa wanadaiwa na kujipatia kiasi cha Sh. 2,700,000/= na kuifanya mali yao binafsi bila kuiweka katika akaunti ya Kijiji.
Washtakiwa walikiri makosa yote yanayowakabili na Hoja za Awali (PH) zikasomwa mbele ya washtakiwa.
Hata hivyo washtakiwa walipopewa nafasi ya kujitetea, ilibainika wameshalilipa deni lao lote la Sh. 2,700,000/= katika akaunti ya Kijiji cha Mago na Jamhuri ikashinda kesi kwa Hakimu kuwapa adhabu washtakiwa wote wawili ya kifungo cha nje (Conditional Discharge) cha miezi 24.
TAKUKURU, Makete-Aprili 11, 2025.