MTENDAJI WA KIJIJI CHA CHISENGA, HALMASHAURI YA WILAYA YA KALAMBO HATIANI KWA MAKOSA RUSHWA NA UHUJUMU UCHUMI

Aprili 10, 2025, Mahakama ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa imemtia hatiani Bw. Edwin Pascal Umella(56) Mtendaji wa Kijiji cha Chisenga kwa makosa ya Ubadhirifu na ufujaji, kinyume na kifungu cha 28(1) na matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 marekebisho ya mwaka  2022 vikisomwa pamoja  aya  ya 21 jedwali la kwanza na kosa la kuisababishia hasara mamlaka kinyume na aya ya 10(1) chini ya kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa sura 200 marekebisho ya mwaka 2022.
Shauri hilo la Uhujumu Uchumi namba 4669/2025 limesikilizwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kalambo Mh. Nickson K. Temu na Wakili wa Serikali kutoka TAKUKURU (M) Rukwa Bw. Mohamed Kassim.
Mshtakiwa amehukumiwa kulipa faini ya sh. 750,000/= na amerejesha fedha zote kiasi cha sh. 1,696,100/= alizofanyia ubadhirifu.
 TAKUKURU RUKWA, Aprili 10, 2025.

Taarifa kwa Umma