Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Crispin Francis Chalamila, amepokea Viongozi na Wanafunzi 100 kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa – (National Defense College – NDC) cha Jijini Dar es Salaam.
Wageni hawa wakiongozwa na Brigedia Jenerali Charles Ndiege – Senior Directing Staff, wamefika TAKUKURU Machi 12, 2025 kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye alitoa wasilisho kuhusu Umuhimu wa TEHAMA katika kuimarisha Ulinzi wa Taifa ambapo alifafanua namna TAKUKURU inavyotekeleza majukumu yake kwa kutumia TEHAMA ili kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.
Aidha, wakiongea na waandishi wa habari baada ya mafunzo hayo, Brigedia Jenerali Charles Ndiege aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuimarisha mapabano dhidi ya Rushwa nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin Francis Chalamila alitoa wito kwa wananchi kuepuka kuomba rushwa kwa wagombea na kwa wagombea kutotoa rushwa wakati nchi ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu, kwani kufanya hivyo kutakwamisha zoezi la kuwapata viongozi safi na walio bora. “Kupokea rushwa kunaondoa haki ya kudai maendeleo”, alisisitiza Bw. Chalamila.
Mkurugenzi Mkuu alisema TAKUKURU imeanza kutoa elimu kwa viongozi wa dini pamoja na makundi mbalimbali kwenye jamii kuhusu athari za rushwa wakati wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha wajibu wao wa kushirikiana na Serikali katika Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Ziara hiyo ya mafunzo ya wanafunzi kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa – hufanyika kila mwaka kwa kutembelea Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo TAKUKURU ili kujijengea uwezo.