Januari 14, 2025. Afisa MISITU wa Jumuiya ya uhifadhi msitu wa SULEDO *Bw. SILOMA MANYINDO MTERO* amefikishwa mahakamani na kufunguliwa shauri la jinai namba 03/2025 kwa makosa ya kuomba na kupokea Rushwa kinyume na k/f cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, pamoja na kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na k/f cha 302 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Mshtakiwa huyo aliomba Rushwa kiasi cha shilingi 600,000 kutoka kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ndilali ili awaruhusu baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho kufanya shughuli za kilimo ndani ya msitu wa SULEDO.
Shauri tajwa limesomwa mahakamani na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wakili YAHAYA MASAKILIJA mbele ya Mhe. ARON LOSIOKI – Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kiteto.
Mshtakiwa amesomewa hati ya mashtaka na amekana mashtaka yote yanayomkabili, lakini amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana.
Shauri hili limepangwa tarehe 28.01.2025 kwa ajili ya kusikilizwa hoja za awali (PH).
TAKUKURU – KITETO JANUARI 14, 2025.