WAWILI WAHUKUMIWA MIAKA 20 JELA KWA KUHUJUMU MAPATO YA HALMASHAURI YA WILAYA YA UKEREWE

MAHAKAMA ya Wilaya Ukerewe imewahukumu waliokuwa Mawakala wa kukusanya mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Bw. PETER MUGONO CASTORY (48) na Bi. ESTHER DOMINIC MAGESA(34) kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya Ufujaji na Ubadhirifu pamoja na Matumizi mabaya ya mamlaka, kinyume na vifungu vya 28 (1) pamoja na 31 vyote vya  Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  [CAP 329 R.E 2022], vikisomeka pamoja na Aya ya 21, Jedwali la kwanza, pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) na (3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 toleo la Mwaka 2022.
Hukumu dhidi ya Bw. PETER MUGONO CASTORY na Bi. ESTHER DOMINIC MAGESA  imetolewa Disemba 4, 2024 kutokana na mashauri ya Uhujumu Uchumi Na. 39594 na 520846 ya mwaka 2023  yaliyokuwa katika Mahakama ya Wilaya Ukerewe mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu LUCAS NYAHENGA, mashauri ambayo yaliendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza – Wakili MOSES MALEWO.
Awali ilielezwa kuwa Washtakiwa hao  walifikishwa Mahakamani hapo kwa mashtaka tajwa hapo juu kwa Bw. PETER MUGONO CASTORY kushindwa kuwasilisha kiasi cha sh 8,529,122.64 na Bi. ESTHER DOMINIC MAGESA sh 8,441,284.29 katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe fedha ambazo kwa nyakati tofauti walizikusanya kutoka kwenye vyanzo mbali mbali vya mapato vya Halmashauri hiyo huku wakijua ni kinyume na  Memoranda ya Fedha za Halmashauri za mwaka 2009 lakini pia Kinyume na Sheria ya Fedha za Halmashauri sura ya 290 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019, ambapo Sheria hizi zote  zilimtaka kila mmoja  alipokusanya mapato ya Halmashauri kuyawasilisha kwenye akaunti ya Halmashauri kila siku anapokusanya ama kesho yake endapo kuna changamoto.
Sambamba na kifungo cha miaka ishirini jela (20), kila mmoja ametakiwa kurejesha kiasi anachodaiwa  katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza.

Taarifa kwa Umma