MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya imemhukumu aliyekuwa mratibu wa huduma za maabara Mkoa wa Mbeya wa Taasisi ya Henry Jackson Faundation Medical Research International (HJFMRI) Bw Emmanuel Tumainiel Malewo adhabu ya kulipa faini ya sh. 500,000/= au kutumikia kifungo cha miaka 3 jela kwa kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Hukumu hiyo iliyotokana na shauri la jinai Na. 33635/2024 ilitolewa Novemba 29, 2024 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Bw Scout Andrew, kesi iliyokuwa ikiendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Sospeter Tyeah.
Ilielezwa kuwa Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa shtaka la kuomba na kupokea Rushwa kutoka kwa walalamikaji waathirika ambao aliwashawishi wampatie kiasi cha sh. 15,153, 000/= ili asiwaondoe kufanya kazi ya kusafirisha sampuli za damu za binadamu kutoka kwenye vituo mbali mbali katika Wilaya ya Mbarali kwenda kwenye maabara ya Hospitali ya Wilaya ambapo ni kinyume na taratibu, kanuni na taratibu.
Kitendo hiki ni kinyume na k/f. 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Emmanuel amelipa faini yote sh. 500,000/= na amerejesha kwa waathirika husika – kiasi cha sh. 15,153,000/=alichopokea toka kwa waathirika hao.