MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya imemhukumu aliyekuwa Meneja wa Majanga wa Tanzania Red Cross Society Bi Magreth Daniel Lugata, adhabu ya kutofanya kosa lolote la jinai ndani ya miezi 6 kwa kosa la ubadhilifu kinyume na kifungu cha 28 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007(CAP 329 R.E 2022).
Hukumu dhidi ya Mshtakiwa huyo Bi Magreth Daniel Lugata katika shauri la jinai Na. 38221/2023 ilitolewa Novemba 28, 2024 na Hakimu Mkazi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Bw Scout Andrew, kesi iliyokuwa ikiendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Sospeter Tyeah.
Ilielezwa kuwa Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa shtaka la ubadhilifu wa sh. 700,000/= fedha alizokabidhiwa afanye malipo kwenye mafunzo ila yeye akazitumia kwa manufaa yake binafsi na kughushi nyaraka akionesha amewalipa watu kwenye mafunzo hali akijua kuwa sio kweli.
Hukumu hii imetokana na makubaliano (plea bargaining agreement) kati ya DPP na mshtakiwa baada ya mshtakiwa kumtaarifu DDP kuwa ana nia ya kukiri makosa yake.
Aidha kutokana na makubaliano kwenye plea bargain mshtakiwa alilipa hasara na fidia ya kiasi cha sh 2,000,000/= kwenye akaunti ya DPP Iliyopo Benki Kuu ya Tanzania.