MAHAKAMA ya Wilaya ya Chunya imemtia hatiani Afisa Tabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya Bw Lazari Kwilasa na kisha kumpatia adhabu ya kulipa faini ya sh. 500,000/= au kutumikia kifungo cha miaka 3 jela, kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya sh. 60,000/= kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Hukumu dhidi ya Afisa Tabibu Lazaro Ernest katika shauri la jinai Na. 27730/2024 ilitolewa Novemba 26, 2024 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya Mhe.James Mhanusi kesi iliyokuwa ikiendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Sospeter Tyeah.
Ilielezwa kuwa Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani kwa shtaka la kuwashawishi walalamikaji wampatie kiasi cha sh. 60,000/= ili aweze kuwapatia matibabu.
Walalamikaji walimpatia Tabibu Lazaro fedha hiyo kinyume na taratibu kwani hakustahili kupokea hongo, hivyo ni kosa la kupokea rushwa k/f.15(1)(b) cha sheria ya kuzuia na kupambana rushwa namba 11 ya 2007.
Mahakama katika hukumu yake imemkuta mshtakiwa na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Tshs laki tano (500,000) ambazo mshitakiwa amelipa faini hiyo.
Mahakama pia ilimuamuru mshtakiwa kurejesha fedha sh. 60,000/= alizopokea awali .