MAHAKAMA ya Wilaya Ukerewe imemhukumu aliyekuwa Wakala wa kukusanya mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe JOSEPH PALAPALA NKOLONGO mwenye umri wa miaka 28, adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Mshtakiwa amekutwa na hatia katika makosa ya Ufujaji na Ubadhirifu pamoja na Matumizi Mabaya ya Mamlaka kinyume na vifungu vya 28 (1) pamoja na 31 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [CAP 329 R.E 2022], vikisomeka pamoja na Aya ya 21, Jedwali la kwanza, pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) na (3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Toleo la Mwaka 2022.
Hukumu dhidi ya Bw. JOSEPH PALAPALA NKOLONGO imetolewa Novemba 25, 2024 kutokana na shauri la Uhujumu Uchumi Na. 39597/2023 lililokuwa katika Mahakama ya Wilaya Ukerewe mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Lucas Nyahenga na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza Bw. Moses Malewo.
Awali ilielezwa kuwa Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani hapo kwa mashtaka tajwa hapo juu kwa kushindwa kuwasilisha kiasi cha Tsh 16,394,246.92/= katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe fedha ambazo alizikusanya kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato vya Halmashauri hiyo akiwa Wakala wa kukusanya mapato.
Bw. JOSEPH PALAPALA NKOLONGO alifanya hivyo akijua ni kinyume na Memoranda ya Fedha za Halmashauri za mwaka 2009 lakini pia Kinyume na Sheria ya Fedha za Halmashauri Sura ya 290 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019, ambapo Sheria hizi zote zilimtaka kila alipokusanya mapato ya Halmashauri kuyawasilisha kwenye akaunti za Halmashauri
kila siku anapokusanya ama kesho yake endapo kuna changamoto.
Sambamba na kifungo cha miaka ishirini jela, ametakiwa pia kurejesha kiasi cha Tshs 16,394,246.92 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.