UJUMBE WA WATAALAM KUTOKA IMF

Ujumbe wa Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), wameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU kwa jitihada ambazo inaendelea kuzitekeleza katika kuzuia na kupambana na rushwa nchini.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa kikao cha Wataalamu hao na TAKUKURU kilichoongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi. Neema Mwakalyelye.

Wajumbe hao – Bw. Sebastian Acevedo na Bw. Charalambos Tsangarides wapo nchini kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa Programu mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali zenye ufadhili wa mkopo nafuu kupitia dirisha la Extended Credit Facility (ECF).

Kupitia kikao hicho, ilielezwa kuwa pamoja na mambo mengine Tanzania imefanikiwa kujumuisha maudhui ya kuzuia na kupambana na rushwa kwenye somo jipya la HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI, linalofundishwa katika Shule za Msingi, Shule za Sekondari za Chini na Shule za Sekondari za Juu (kwa mujibu wa Mtaala ulioboreshwa Mwaka 2023); Uzinduzi na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Nne – NACSAP IV pamoja na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU Rafiki inayoshirikisha wadau katika kuzuia vitendo vya rushwa.

Pamoja na TAKUKURU, wataalamu hawa wanatembelea Tume ya Mipango, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF.

Taarifa kwa Umma