Wakati Dunia ikishuhudia majanga katika maeneo mbalimbali, Mamlaka za Kupambana na Rushwa ukanda wa SADC zimetahadharishwa kuwa makini kwani mikakati ya haraka inayoandaliwa kukabiliana na hali hiyo inaweza kutoa mianya ya rushwa.
Akizungumza Oktoba 2, 2024 katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa mamlaka hizo jijini Lusaka – Zambia, Mwenyekiti mpya wa Kamati ya SADC ya Kupambana na Rushwa (SADC Anti Corruption Committee – SACC) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini – TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, amefafanua kuwa hatari ya uwepo wa vitendo vya rushwa inaweza kujitokeza wakati wa mchakato wa kupata na au kutoa misaada wakati wa dharura.
“Hatua zote za mnyororo wa utoaji wa misaada ziko katika hatari ya rushwa kutokana na dharura inayokuwepo”, alisema.