TUZINGATIE MAADILI KATIKA UTENDAJI KAZI – NAIBU WAZIRI SANGU

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu, amewataka Watumishi wa TAKUKURU kuzingatia maadili katika utendaji wao wa kazi.

Mhe.Sangu ameyasema hayo Septemba 5, 2024, alipotembelea Ofisi za TAKUKURU Makao Mkuu na kufanya kikao kazi na Watumishi.

Aidha, Mhe. Sangu ameitaka TAKUKURU kudhibiti rushwa katika Ununuzi wa Umma kwa kuwa sehemu kubwa ya Bajeti ya Serikali inaelekezwa kwenye manunuzi.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu Bw. Mululi Mahendeka aliyeambatana na Mhe Naibu Waziri, amewasisitiza watumishi wa TAKUKURU kutunza SIRI kutokana na jukumu nyeti la taasisi hiyo.

“Taasisi hii ni muhimu sana katika usalama wa nchi. Rushwa ikishamiri miongoni mwa jamii usalama wa nchi utatetereka”. Alisema Bw. Mahendeka.

Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin Chalamila aliwashukuru Viongozi hao kwa kufika TAKUKURU na kueleza namna ambavyo TAKUKURU inashirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kutekeleza majukumu yake.

Taarifa kwa Umma