TANZANIA imekuwa mwenyeji wa Kikao Kazi cha 27 cha Kamati Tendaji ya Shirikisho la Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa – Afrika Mashariki.
Kikao hiki kinachofanyika jijini Arusha Septemba 11 – 12, 2024, kinajumuisha Wakuu wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka Uganda, Kenya, Rwanda na Tanzania kwa lengo la kujadili na kubadilishana uzoefu katika jitihada za kuzuia na kupambana na Rushwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Awali, akiwakaribisha wageni hawa, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin Francis Chalamila amesema mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji nguvu za pamoja hivyo kuanzishwa kwa shirikisho hili kumeimarisha mapambano hayo kati ya nchi na nchi na Afrika Mashariki kwa Ujumla.
TAKUKURU ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya EAAACA ambapo Mwenyekiti ni Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Uganda – IGG na Makamu Mwenyekiti ni Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Kenya – EACC.