Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU imendesha Warsha za wadau kwa lengo la kuweka mikakati ya kudhibiti Rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Mwaka 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Warsha hizi zimefanyika PCCB House Upanga Dar Es Salaam ambapo Juni 26, 2024 ilikuwa ni Warsha ya Asasi za Kiraia pamoja na Asasi Zisizo za Kiserikali; Juni 27, 2024 ni Warsha ya Viongozi wa Dini na Juni 28, 2024 ni Warsha na Wahariri wa Vyombo vya Habari.
Akifungua Warsha na Asasi za Kiraia pamoja na Asasi Zisizo za Kiserikali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP. Salum Rashid Hamduni amesema hatua ya kuwashirikisha wadau katika kudhibiti vitendo vya rushwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika bila kuwepo kwa vitendo vya rushwa.
“TAKUKURU inaamini ushiriki wenu wa moja kwa moja katika kuandaa Mkakati wa kudhibiti vitendo vya Rushwa kwenye uchaguzi una faida kubwa kwa Taifa, jamii na mtu mmoja mmoja. Faida hizo ni pamoja na kuchaguliwa kwa viongozi bora watakao ongoza kwa mujibu wa sheria na kutekeleza mipango ya maendeleo’. Alisema Mkurugenzi Mkuu.