RAIS MWINYI AZIPONGEZA TAKUKURU NA ZAECA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezipongeza TAKUKURU na ZAECA kwa kuendelea na ushirikiano wa karibu katika kuzuia vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi.

Rais Mwinyi ameyasema hayo akiwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika 2024 yaliyofanyika Zanzibar Julai 11, 2024.

Rais Mwinyi pia ametoa wito kwa ZAECA na TAKUKURU kuongeza jitihada katika kuwashirikisha wananchi hususan vijana katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi ili waoneshe mchango wao katika mapambano ya vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Kaulimbiu ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Afrika kwa mwaka 2024 inasema: Mifumo Madhubuti ya Ulinzi wa Watoa Taarifa: Nyenzo Muhimu katika Mapambano Dhidi ya Rushwa.

KATIKA HATUA NYINGINE Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye, alipokea TUZO kutoka ZAECA aliyokabidhiwa na Mhe Dkt. Hussein Ali Mwinyi – Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kutambua ushirikiano uliopo kati ya TAKUKURU na ZAECA katika Mapambano Dhidi ya Rushwa.