MHANDISI MANISPAA UBUNGO AFUNGWA JELA MIAKA 20 KWA KUISABIBISHIA MANISPAA HASARA.
Februari 7, 2024 Kesi Namba Ecc 12/2022 imeamuliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni Wilaya ya Kinondoni, ambapo mshtakiwa Bw. Ramadhani Mabula Maige – Aliyekuwa Mhandisi wa Maji Manispaa ya Ubungo na sasa ni Mhandisi wa Maji Wilaya ya Kilwa, amehukumiwa kulipa faini ya shilingi Milioni Mbili (2,000,000/=) au kutumikia kifungo cha miaka miwili (2) jela kwa kosa la kwanza la Matumizi Mabaya ya Madaraka, kinyume na K/F cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 (R.E 2022). Pia mshtakiwa huyo alihukumiwa Kifungo cha Miaka Ishirini (20) jela kwa kosa la Kuisababishia Hasara Mamlaka Kinyume na Aya ya 10 (1) na (4) Jedwali la Kwanza na Vifungu 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 (R.E 2022).
Katika hatua nyingine, Bi. Martha Athanas Ivo aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Mbezi akiwa ni Mshtakiwa wa Pili amekutwa na hatia kwa kosa la Matumizi Mabaya ya Madaraka K/F 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (R.E 2022) na amehukumiwa kwenda jela Miaka Miwili au kulipa faini ya Shilingi Milioni Mbili.
Washtakiwa walitumia madaraka yao vibaya wakati wa kutekeleza Mradi wa Maji Mpigi Magohe kwa kutofuata maelekezo ya kutekeleza mradi huo uliotumia utaratibu wa ‘Force Account’ na hivyo kusababisha hasara ya Shilingi Milioni Nane (8,000,000/=) kwa Manispaa ya Ubungo baada ya mradi huo kushindwa kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Hukumu hiyo imesomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni na Mheshimiwa Jackline Rugemalira na washtakiwa wamepelekwa jela.