Shauri la Uhujumu Uchumi namba 2015/2024- Jamhuri dhidi ya Bw. BONIFACE YOHANA NKAKATISI– Katibu Mkuu Taifa wa CHAMA CHA WAFANYAKAZI WA VIWANDA, BIASHARA-TAASISI ZA FEDHA, HUDUMA NA USHAURI (TUICO) imefunguliwa leo Januari 31, 2024 mbele ya Mh. Bittony Mwakisu (SRM) katika Mahakama ya Wilaya Ilala.
Mshtakiwa ameshtakiwa kwa kosa la kutumia madaraka yake vibaya kinyume na kifungu cha 31 na kosa la Ubadhirifu na Ufujaji wa fedha kiasi cha TZS .238,545, 044/= kinyume na kifungu cha 28 (2) vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 329 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200,R.E 2022.
Mshtakiwa amekana makosa yote na kupelekwa mahabusu baada ya kutokukidhi masharti ya dhamana.
Kesi imeahirishwa hadi tarehe 05.02.2024 kwa ajili ya kutajwa.
Aidha Shauri lingine la Uhujumu Uchumi namba 2438/2024 – Jamhuri dhidi ya Jackson Moses Ngalama -Chief Executive Director TALGWU, Emmanuel Gilbert Mdoe -Accountant TALGWU, Pamela Miguna Sellemia – Head of Loan Department TALGWU, Timothy Peter Mashishanga – Dereva imefunguliwa leo Januari 31, 2024 mbele ya Mh. Rehema Lyana (RM).
Washtakiwa wameshtakiwa kwa makosa ya; Matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31, kusaidia kutenda kosa kinyume na kifungu cha 30 na kosa la Ubadhirifu na Ufujaji wa fedha kiasi cha TZS.133,584,000/= kinyume na kifungu cha 28(2) vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 329 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 R.E 2022.
Washtakiwa wamekana makosa yote na kurejeshwa mahabusu kwasababu wanakabiliwa na kesi nyingine ambayo haina dhamana.
Kesi imeahirishwa hadi Februari 14, 2024 kwa ajili ya kusoma Hoja za Awali.