Afisa Mtendaji wa Kata ya Sagata kizimbani kwa ubadhirifu wa kiasi cha Sh. 1,628,000/=
Afisa Mtendaji wa Kata ya Sagata katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Bw. SOLOMON DUNGA MBISE, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu kwa mashtaka manne;
- Ubadhirifu na ufujaji
- Matumizi mabaya ya madaraka
- Kusababishia hasara Mamlaka
- Wizi kwa Mtumishi wa Umma wa kiasi cha Shilingi 1,628,000/= fedha za mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Itilima alizokusanya kwa kutumia mashine za POS.
Akisoma mashtaka hayo katika kesi na. ECO 06/2023 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Mhe. Robart Kaanwa, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Bw. Bahati Kulwa akisaidiana na Bw. Edgar Mkumbo na Wisley Ngwembe, alisema makosa hayo ni kinyume na Kifungu cha 28(1) cha PCCA, kifungu cha 31 cha PCCA kikisomwa pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha EOCCA, Kifungu cha 265 na 270 cha Penal Code.
Baada ya kusomewa makosa hayo, mshtakiwa alikana makosa yote. Pia mshtakiwa aliijulisha mahakama kuwa ana nia ya kufanya mazungumzo ya Plea Bargaining na ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Simiyu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 19, 2024 ili mshtakiwa aweze kukamilisha hatua za Plea Bargaining na ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Simiyu.
Mshtakiwa alifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo yupo nje kwa dhamana.
TAKUKURU Simiyu. Disemba 20, 2023