Afisa Tabibu kizimbani kwa kuomba na kupokea hongo ya TSh. 150,000/=
Afisa Tabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Bw. Msafiri Omary Kalomo, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida kwa shtaka la kuomba na kupokea hongo ya TSh. 150,000/= kutoka kwa Bi. Neema Msengi Kilimba ili amsaidie kufanya upasuaji wa uvimbe katika tumbo la uzazi.
Akisoma mashtaka katika kesi hiyo namba CC. 01/2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Luzango Khamsini, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wakili Yvonne Munisi, alisema kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) & (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329 Marejeo ya Mwaka 2022.
MSHTAKIWA ALIKANA MAKOSA HAYO na kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 18, 2024 ambapo mshtakiwa atasomewa hoja za awali.