Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU CP. Salum Rashid Hamduni pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni – BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, wamesaini MKATABA WA USHIRIKIANO WA KIKAZI (MoU) baina ya taasisi hizi mbili. Mkataba huu unalenga kutia nguvu na kurasimisha ushirikiano wa taasisi hizi mbili kwa maeneo yaliyokubaliwa na pande zote mbili, ambayo ni pamoja na: (i) Kubadilishana taarifa za kiuchunguzi kwa lengo la kupata ushahidi utakowezesha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani; (ii)Kuimarisha mfumo na utaratibu wa mafunzo kwa watumishi wa BRELA kuhusu dhana ya Rushwa, madhara yake na namna watumishi hao wanavyoweza kupambana na rushwa ndani ya BRELA , pamoja na (iii) Kushirikiana katika kufanya utafiti na tathmini ya mifumo ya kiutendaji ndani ya BRELA kwa lengo la kubaini na kuziba mianya ya rushwa ndani ya BRELA.
Tukio hili limefanyika Desemba 7, 2023 katika ofisi za Makao Makuu ya BRELA yaliyoko Jijini Dar Es Salaam.