Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Mufindi pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mapanda kizimbani kwa ubadhirifu wa zaidi ya Sh. Milioni 19
Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Wilaya ya Mufindi Bw. Jeswald Gustav Ubisiambali na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mapanda Bw. Oberd Francis Madembo, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kwa mashtaka mawili;
- Ubadhirifu na ufujaji
- Wizi akiwa Mtumishi wa Umma wa kiasi cha Shilingi 19,970,000/= mali ya Kijiji cha Mapanda kilichopo Wilaya ya Mufindi.
Akisoma Mashtaka hayo katika kesi na. ECO 15/2023 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Mhe. Edward Uphoro, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Bi. Restituta Kessy akisaidiana na Bi. Husna Kyoba na Bi. Lisa Gwakisa Kasongwa, alisema makosa hayo ni kinyume na Kifungu cha 28(1) cha PCCA na Kifungu cha 258(1) na (2) Na. 270 cha Penal Code.
Washtakiwa walikana makosa yao na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 13, 2023 ambapo washtakiwa watasomewa hoja za awali.
Washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa mahabusu.