Askari Wanyamapori, Mfanyabiashara wa Mbao na Mjasiriamali, kizimbani kwa kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania hasara ya kiasi cha Shilingi 2,231,000/=
Askari Wanyamapori Bw. Ibrahim Silas Mtaki, Mfanyabiashara wa mbao Bw. Roden Esches Mwalongo na Mjasiriamali Bi. Lilian John Jombe, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kwa shtaka la kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania hasara ya kiasi cha Shilingi 2,231,000/=.
Akisoma mashtaka hayo katika Kesi na. ECO 14/2023 mbele ya Hakimu Mkazi wa wilaya hiyo Mhe. Edward Uphoro, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Bi. Restituta Kessy akisaidiana na Bi. Husna
Kyoba na Bi. Lissa Gwakisa Kasongwa alisema makosa hayo ni Kinyume na Aya ya 10 ya Jedwali la kwanza na Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Mshtakiwa wa kwanza Bw. Ibrahim Silasi Mtaki na Mshtakiwa wa tatu Bi. Lilian John Jombe walisomewa mashtaka yao ambapo mshtakiwa wa kwanza alikana na Mshtakiwa wa tatu alikiri na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.
Mshtakiwa wa pili hakufika mahakamani kwa sababu za ugonjwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 13, 2023 ambapo washtakiwa watasomewa hoja za awali.