Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, amefungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU 2023 Jijini Dodoma. Akiongea wakati wa ufunguzi Mhe. Simbachawene amewataka Viongozi wa TAKUKURU kujadili changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi na kuzifanya kuwa fursa kwa maendeleo ya Taifa. “Ninaamini mtatumia fursa ya mkutano huu kujadili masuala yote yanayoonekana kuwa ni changamoto katika utendaji kazi ili kupata suluhu ya pamoja”. Alisema Mhe. Simbachawene. Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa, TAKUKURU inatakiwa kuitumia vizuri Programu TAKUKURU Rafiki ili kupanua wigo wa kuwashirikisha wananchi katika kupambana na rushwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Salum Rashid Hamduni amesema TAKUKURU inaendelea na utekelezaji wa shughuli zake kwa mujibu wa Sheria na sasa wamejikita zaidi katika kuzuia rushwa. “Tunaendelea na kazi ya kuelimisha umma kuhusu masuala ya rushwa na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Serikali ambapo tumeokoa fedha nyingi ambazo kama isingekuwa TAKUKURU basi fedha hizo zingeishia mikononi mwa watu binafsi…”. Amesema CP. Hamduni.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubainisha changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi wao na kutafuta ufumbuzi wa pamoja. Kwa Mwaka 2023 Mkutano huu utahitimishwa Novemba 22, 2023.