Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George B. Simbachawene ametembelea na kukagua Mradi wa Ujenzi wa Jengo la TAKUKURU Makao Makuu lililopo Jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Waziri Simbachawene amepongeza jitihada kubwa zinayofanywa na Mkandarasi SUMA JKT licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza na kuagiza KAZI IENDELEE KWA KASI.
Mhe. Waziri amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaiwezesha TAKUKURU kutimiza kwa ufanisi majukumu yake ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na kufanya rasilimali za Watanzania ziwe salama. “Viongozi tunajivunia kuona ushirikiano uliopo kati ya TAKUKURU, SUMA JKT pamoja na TBA hivyo tuendelee na ukamilishaji wa hatua iliyobaki ili jengo hili likamilike kwa wakati na kwa kiwango kizuri”. Alisisitiza Mhe. Waziri.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Salum Rashid Hamduni amempongeza Waziri kwa kazi kubwa ya kuisemea taasisi Bungeni na amemshukuru Mhe. Waziri kwa kutembelea jengo hili jambo ambalo amesema linazidi kutoa hamasa kwa Watumishi wa TAKUKURU. Mradi wa ujenzi wa Jengo la TAKUKURU Makao Makuu unatarajiwa kukamilika Julai 2024.