Novemba 7, 2023 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Manyara imemfikisha Mahakamani Bw. IDDI ISSA RULAMYE – Mpima Ardhi Msaidizi aliyekuwa Halmashauri ya Mji Babati na Wenzake Wawili.
Washtakiwa hao wamefikishwa mbele ya Mh. MARTINE MASAO Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Manyara kwa makosa ya kutumia madaraka vibaya na kumilikisha ardhi kwa wananchi pasipo kuhusisha Kamati ya Umilikishaji Ardhi; Kughushi; Kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu; Utakatishaji fedha pamoja na Kuisababishia Mamlaka husika hasara ya sh. 84,000,000/=.
Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi imefunguliwa na kusajiliwa kama ECC.No.09/2023 na kusomwa na Wakili wa Jamhuri Bi. EVELINE ONDITI (TAKUKURU) ambapo ameeleza kuwa washtakiwa walikiuka Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya Mwaka 2019 kikisomwa pamoja na Aya ya 21 Jedwali la Kwanza ya Kif. 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 marejeo ya 2019.
Washtakiwa Wengine ni ; JULIAN ANSBERT RUBUKA – Afisa Ardhi na JOSEPH JOHN SELUKELE – Afisa Ardhi Msaidizi.
Mshtakiwa wa kwanza amekosa dhamana kwa vile anashtakiwa kwa kosa la utakatishaji fedha kinyume na kifungu cha 12(a) & 13(1)(a) ya utakatishaji fedha Sura ya 423 Marejeo ya 2019 kikisomwa pamoja na Aya ya 21 Jedwali la Kwanza ya Kifungu cha 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 marejeo ya 2019.
Aidha mshtakiwa wa pili na wa tatu wamepata dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana.
Kesi imepangwa kwa usikilizwaji wa awali Novemba 23, 2023 baada ya wakili EVELINE ONDITI kuieleza Mahakama kuwa uchunguzi wa shauri hili umekamilika.
TAKUKURU, Babati – Manyara. Novemba 8, 2023