Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi. Neema Mwakalyelye amepokea ugeni wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar Mhe. Mgeni Jailani Jecha, ambaye Novemba 7, 2023, ameitembelea TAKUKURU kwa lengo la kutambuana na kupata uzoefu wa kiutendaji. Akizungumza katika kikao kazi pamoja na ugeni huu, Naibu Mkurugenzi Mkuu ameeleza majukumu ya TAKUKURU kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 pamoja na ushirikiano wa kiutendaji uliopo kati ya TAKUKURU na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Naibu Mkurugenzi Mkuu ametaja mafanikio ya ushirikiano kati ya TAKUKURU na DPP kuwa ni pamoja na: -Wanasheria wa TAKUKURU kupewa vibali vya kuendesha mashauri mahakamani; Ugatuzi wa madaraka kwa ofisi za Taifa za Mashtaka ngazi ya mikoa; Kuanzishwa kwa UTATU ambao ni ushirikiano kati ya TAKUKURU, POLISI na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka; Uanzishwaji wa Jukwaa la Haki Jinai pamoja na kuandaliwa kwa kushirikiana – miongozo mbalimbali inayosaidia katika chunguzi za makosa ya rushwa. Kwa upande wake DPP Zanzibar amepongeza ushirikiano uliopo kati ya TAKUKURU na DPP Tanzania Bara na kuahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa upande wa Zanzibar kupitia Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar – ZAECA. DPP Zanzibar ameambatana na Naibu DPP Mhe. Mwanamkaa Mohammed, Bw. Said A. Said Wakili wa Serikali Mwandamizi pamoja na Bw. Issa S. Ahmed ambaye ni Wakili wa Serikali.