Novemba 6, 2023, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kagera imemfikisha Mahamani Bw. Sunday Augustino Alexander- Afisa Ugavi wa Manispaa ya Bukoba na wenzake wanne.
Washtakiwa hao wamefikishwa mbele ya Mhe. Andrew Kabuka Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Bukoba, kwa makosa ya kutumia madaraka vibaya na kujihusisha na shughuli za mazao ya misitu pasipo kibali cha Mkurugenzi wa Misitu.
Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi imefunguliwa na kusajiliwa kama Ecc. No. 1/2023 na kusomwa na Wakili wa Jamhuri Kelvin Anord Murusuri (TAKUKURU), ambapo ameeleza washtakiwa walikiuka kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya Mwaka 2019 kikisomwa pamoja na Aya ya 21 Jedwali la Kwanza na kif cha 57(1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 marejeo ya 2019.
Washtakiwa wengine ni
- Mchumi wa Manispaa ya Bukoba Bw. Deusdedith Rwekanwa Joseph;
- Mfanyabiashara wa misitu Bw. Julias Kyabwishukuru Rwabande,
- Mfanyabiashara wa misitu Bi. Adelina Revelian Kitare na
- Mfanyabiashara wa misitu Bi. Consolatha John Balole.
Pia kwa Wafanyabiashara wa misitu Wakili Murusuri ameieleza Mahakama kuwa wafanyabiashara wote wanatuhumiwa pia kukiuka Sheria ya Misitu kwa kujishughulisha na misitu isivyo halali hivyo kuenenda kinyume na kif cha 89(d) na 97(b) vikisomwa pamoja na Aya ya 33 ya Jedwali la Kwanza vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Mapitio ya 2019.
Washitakiwa wote wamekana makosa yao na kupatiwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana.
Kesi imepangwa kwa usikilizaji wa awali tarehe 24/11/2023 baada ya Wakili Murusuri kuieleza Mahakama kuwa Upelelezi wa shauri hili umekamilika.