Novemba 3, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya mbele ya Mhe Mtengeti Sangiwa, imeamuliwa Kesi ya Jinai na 215/2022, Jamuhuri dhidi ya
Lambert Haule ambaye ni Afisa Mionzi katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya.
Mshitakiwa huyo ameshtakiwa kwa kosa la kujipatia fedha kiasi cha sh. 1,000,000 /= kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Bi. Paulina Mbezi akidai kuwa atamsaidia kuongea na Maafisa wa TAKUKURU (M) Mbeya wasiendelee na uchunguzi wa makosa ya Rushwa unaoendelea dhidi yake.
Jambo hili lilikuwa ni la udanganyifu kwani Bi. Paulina Mbezi hakuwa na tuhuma za rushwa zilizokuwa zinachunguzwa na TAKUKURU (M) Mbeya.
Kosa hili ni kinyume na vifungu vya 301 na 302 vya Kanuni ya Adhabu [CAP 16 R.E 2022] pamoja na kifungu cha 28 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007.
Mashtakiwa ametiwa hatiani kwa kosa hili na amehukumiwa kulipa faini ya sh 500,000/= au kwenda jela miaka 3.