Oktoba 3, 2023 katika Mahakama ya Wilaya Muleba mbele ya Mhe Lilian Mwambeleko, imeamuliwa kesi ya Jinai na. 91/2023, Jamhuri dhidi ya Adilelius Vedasto Apolinary.
Adilelius ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi cha ujasiriamali cha ‘Umoja wa Vijana Youth Fund’ kilochopo Muleba, alishtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uwongo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuhusu matumizi ya sh. Milioni 60 ambazo zilitolewa na Halmashauri ya Muleba Mwaka 2022 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana.
Kosa hili ni kinyume na kif cha 122 cha Kanuni za Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya 2022.
Kesi hii iliongozwa na Wakili Kelvin Murusuri kutoka TAKUKURU na mshtakiwa ameamriwa alipe faini ya sh. Laki tano 500,000/- au kutumikia kifungo cha miezi sita jela. Pia kufuatia maombi ya Wakili Murusuri mshtakiwa huyo ameamriwa arejeshe fedha zote sh. Milioni Sitini ndani ya miezi mitatu na tayari amelipa sh. Milioni Tisa katika akaunti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Muleba.