Mshtakiwa huyo ambaye ni Karani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Archileus Anatory Rutayangurwa amefunguliwa shauri la Rushwa Na. 09/2023 Septemba 21, 2023, katika Mahakama ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, mbele ya Hakimu Mhe. Lilian Mwambeleko.
Mshtakiwa amesomewa mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya rushwa chini ya kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2022 pamoja na kutokutii wajibu wa kisheria chini ya kifungu cha 123 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2022.
Inashtakiwa kwamba kati ya Januari 2018 na Desemba 2019, kwa njia ya udanganyifu mshtakiwa alijipatia kiasi fedha Sh. 3,116,300/= mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Muleba aliyoikusanya kupitia mashine ya POS.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana na shauri litakuja tena Oktoba 18, 2023.
Upande wa Jamhuri katika Shauri hili unawakilishwa na Wakili Daudi Jocob Oringa kutoka TAKUKURU.