Maafisa Biashara hao Richard Lubega Kubona, Adelina Kasigwa Leonard na Musa Said Kalumba, wamefunguliwa Kesi ya Uhujumu Uchumi (ECO. Na. 07/2023) Septemba 20, 2023, katika Mahakama ya Hakimu Mkaazi Bukoba Mkoani Kagera, mbele ya Hakimu Mfawidhi Mhe. Janeth Massesa.
Washtakiwa wote wamesomewa makosa ya kutumia madaraka vibaya, ubadhirifu, ufujaji pamoja na matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri, Kinyume na vifungu vya 22, 28 na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Cap 329 R.E 2022), vikisomwa pamoja na vifungu vya Uhujumu Uchumi Aya ya 21 jedwali la kwanza, kifungu cha 57 (1) na 60 (2) Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2022.
Pia walisomewa shtaka la Utakatishaji Fedha Shs Milioni Mia Nne na Tisa Laki Nne Tisini na Saba Mia Moja Sitini na Tano (sh. 409,497,165/-), mali ya Manispaa ya Bukoba – Kinyume na kifungu cha 12 (1)(d) na 13 (1)(a) vya Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Sura ya 432 Marejeo ya 2022, vikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi Aya ya 22 Jedwali la Kwanza na kifungu cha 57(1) na 60 (2).
Mengine ni Kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335 (a) na 337 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 Mapitio ya 2022.
Kosa lingine ni kuisababishia mamlaka (Manispaa ya Bukoba) hasara, kinyume na Aya ya 10 (1) Jedwali la Kwanza na kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 Mapitio ya 2022
Wanashtakiwa kwa makosa hayo kwa kukusanya mapato ya Manispaa ya Bukoba na kufuja kwa manufaa yao, huku wakidanganya kuwa jumla ya Sh 409,497,165/- ziliwekwa katika Benki ya NMB Bukoba akaunti ya Manispaa, huku wakijua kuwa ni uwongo.
Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama ile haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo wamepelekwa rumande hadi Oktoba 4, 2023 litakapotajwa tena.
Shauri hili linaendeshwa na Wakili Kelvin Murusuri akisaidiana na Jacob Daudi kutoka TAKUKURU.