Agosti 28, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, limefunguliwa shauri la Uhujumu Uchumi Namba 03/2023 dhidi ya ROBERT ANDREW MPELETA (Mfanya biashara), ANORD JIFIKE NZALI (Mfanya biashara), ISAYA ANDEMBWISYE GERALD (Mwalimu), BWIGANE SETH MWAMELO (Mtendaji wa Kijiji), PETER JOSEPH MANGALI (Mkusanya Ushuru), BENEDICT SALVATORY MILLINGA (Afisa Tehama H/W Mbeya DC), ZUELI ABASI MKWAMA (Mkusanya Ushuru), KHALID ABDALLAH HABIBU (Mkusanya Ushuru), FADHIL FRED LWESYA (Mkulima), SHUKURU SIMBEYE (Mkusanya Ushuru), DANIEL MTWEVE (Mkusanya Ushuru), EZEKIA ADAM MWAISUNGA (Mkusanya Ushuru), TALIKI PAULO SAMSON (Mkusanya Ushuru), na ULIMBOKA ADAMSON (Mkusanya Ushuru).
Washtakiwa kwa pamoja wameshitakiwa kwa kosa la Kuendesha Genge la Uhalifu kinyume na Aya ya 4(1)(a) ya Jedwali la Kwanza pamoja na Kifungu cha 57(1) na 60(1) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Kwamba, washitakiwa hawa wametenda kosa hili mara baada ya kutengeneza mfumo haramu wa kukusanya ushuru wa mazao katika H/W Mbarali, H/W Rungwe, H/W Mbeya DC, H/w Ileje na H/W ya Momba na kufanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi 382,764,200/=.
Pamoja na shtaka hili Mshitakiwa wa Nne hadi Mshitakiwa wa Kumi na Nne wameshitakiwa pia kwa kosa la Kumiliki Kifaa Haramu kinyume na Kifungu cha 10(1)(a) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Washitakiwa hawa wameshtakiwa kwa kosa hili kwa kitendo chao cha kukutwa wakimiliki mashine za POS ambazo zilikuwa na mfumo haramu wa kukusanyia ushuru wa mazao.
Mashine hizi walizokutwa nazo ndizo zilizotumika katika utendaji wao wa ukusanyaji wa ushuru kinyume na utaratibu.
Aidha Mshtakiwa wa Kwanza, Tatu na Kumi na Nne wameshtakiwa pia kwa makosa ya Utakatishaji Fedha kinyume na Kifungu cha 12(b) na 13(1)(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha. Makosa haya ya utakatishaji fedha yamefanywa na washtakiwa hawa baada ya kutumia fedha walizozipata kutokana na kukusanya ushuru wa mazao kwa njia haramu kununulia viwanja na nyumba ili kuficha ukweli juu ya uchafu wa pesa husika.
Washtakiwa hawa baada ya kusomewa mashtaka haya hawakupaswa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hii bado haijapewa mamlaka ya kusikiliza shauri hili na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Washitakiwa wote wamekosa dhamana kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa shauri la uhujumu uchumi ambalo kiasi cha fedha inayotuhumiwa ni zaidi ya sh. Milioni 300.
Washitakiwa wote wamerudishwa rumande na kesi itatajwa tarehe 11/09/2023.