Agosti 31, 2023, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imesomwa hukumu ya Shauri la Uhujumu Uchumi ECC. 05/2022 lililowahusu Washtakiwa watatu ambao ni Dkt. John Marco Pima,
- Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha,
Bi Mariam Shabani Mshana – Aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji la Arusha na
Bw. Innocent Gitubabu Maduhu – Aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango wa Jiji la Arusha.
Washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na makosa matatu chini ya Vifungu vya 22, 28(i), na 31 vya PCCA No. 11/2007, makosa mawili chini ya vifungu vya 12 na 13 vya Sheria ya Utakatishaji, kosa la kughushi nyaraka chini ya vifungu vya 333,335 na 337 vya Kanuni ya Adhabu, na Kosa la kuisababishia Mamlaka Hasara chini ya aya 10, jedwali la kwanza vifungu vya 57 na 60 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Washtakiwa wote watatu walifikishwa Mahakamani kujibu Makosa waliyotenda baada ya kushirikiana kuandaa nyaraka zilizopelekea hasara kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kiasi cha Shilingi Milioni Mia Moja na Tatu (Tshs. 103,000,000/=) ambapo fedha tajwa walizitumia kwa manufaa yao binafsi.
MAHAKAMA iliwapata washtakiwa wote watatu na hatia na kuwahukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa kila kosa kwa makosa yote.
Sambamba na adhabu hiyo, hukumu hii iliyotolewa na Mh. Sarafina Nsana, Mahakama pia imeamuru kufilisiwa kwa mali ambayo ilithibitika kupatikana kama zao la rushwa.