Julai 4, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma – PPRA Bw. Eliakim Maswi, wamesaini Mkataba wa Makubaliano ya Kikazi (MoU) baina ya Taasisi hizi, yenye lengo la kuongeza wigo na nguvu ya kukabiliana na tatizo la rushwa katika Ununuzi wa Umma. Akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari mara baada ya utiaji wa saini, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ametaja maeneo ya ushirikiano kati ya TAKUKURU na PPRA kuwa ni: Katika kupeana taarifa za Ki-Uchunguzi na kuchunguza vitendo vya rushwa katika Ununuzi wa Umma; Kupeana taarifa za Ki-Intelijensia kuhusu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa; Kufanya tafiti za kubaini viashiria vya rushwa na kuweka mikakati ya kuvidhibiti pamoja na kuendesha mafunzo yatakayowezesha utambuzi wa Rushwa katika Ununuzi wa Umma .