Juni 26, 2023, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Tanga, Mbele ya Mh. Sophia Salim Masati – Hakimu Mkazi, imefunguliwa kesi ya Uhujumu Uchumi Nambari Ecc.09/2023, Jamhuri dhidi ya;
(a) William John Nguruko, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mabokweni;
(b) Sudi Sungura Mshamu, Karani wa Fedha wa Shule ya Msingi Mabokweni;
(c) Mwanabakari Saidi Athumani-Mjumbe wa Kamati ya Shule ya Msingi Mabokweni;
(d) Yusufu Constantine Mushi, Mwalimu Shule ya Msingi Saruji na
(e) Herieth Audax Mwiki ambaye ni Mke wa Sudi Sungura Mshamu.
Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakamani kwa makosa 33 ya Rushwa na Uhujumu Uchumi yakiwa ni pamoja na Ubadhilifu na Ufujaji wa Fedha Kiasi Cha Sh.28,382,565/=, kinyume na Kifungu cha 28 (1) na (2) Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2022, ikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza na Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2022, Kula Njama kutenda Makosa ya Rushwa kinyume na Kifungu cha 32 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2022, ikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la Kwanza na Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2022, Makosa ya kughushi Kinyume na Kifungu Cha 333, 335, 337 na 338 na 340 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2022 pamoja na Kuisababishia Mamlaka iliyoainishwa Kisheria Hasara ya Sh 28,382,565/= kinyume na aya ya 10(1) jedwali la Kwanza na Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2022.
Kati ya Washtakiwa hao, William John Nguruko na Mwanabakari Saidi Athumani, walikana makosa yote. Yusufu Constantine Mushi alikiri au alikubali kosa la Kujipatia Manufaa ya Sh.16,066,540/= kinyume na Kifungu cha 23 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2022, ikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la Kwanza na Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya Mwaka 2022 na pia Mshtakiwa Sudi Sungura Mshamu alikiri au alikubali Makosa yote 32 kama alivyosomewa Hati ya Mashtaka.
Washtakiwa walitenda makosa hayo katika utekelezaji Miradi ya Ujenzi wa Madarasa na Vyoo katika Shule ya Msingi Mabokweni.
Washtakiwa wote wamepelekwa rumande kufuatia wenzao Sudi Sungura Mshamu na Yusufu Constantine Mushi kuomba kusomewa mashitaka upya ili wajibu upya, kwa madai kwamba waliposomewa mwanzo walikubali bila kuelewa.
Mheshimiwa Hakimu aliahirisha kesi hadi Juni 26, 2023 kwa ajili usikilizwaji wa hoja za awali.