JUNI 23, 2023, Mahakama ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, katika Kesi ya Uhujumu Uchumi Namba 03/2022, imewakuta na hatia SULTAN ALI NASOR na SILVER MAXIMILLIAN MAXIMILLIAN (Wote Maafisa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, (TRA – Kilwa).
Washtakiwa hao wametiwa hatiani kwa makosa ya (1).Matumizi Mabaya ya madaraka k/f cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022,
(2) Kutofanya Tathmini Sahihi ya Kodi k/f cha 7(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Forodha na Tozo Sura ya 403 R.E 2019 na (3)
Kuisababishia Mamlaka Hasara Kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza na vifungu 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya 2022 .
Washtakiwa walifanya tathmini ya kodi kwa madumu ya mafuta ya kupikia 200 tu badala ya 500 ya lita 20 kila moja, mali ya Mfanyabiashara ATHUMANI AHMADI SIMBA .
Mafuta hayo yaliingizwa kutoka Zanzibar kupitia Bandari ya Kivinje kwa Jahazi liitwalo TAWAKAL,
Kitendo cha washtakiwa kutotoza kodi madumu 300 ya mafuta kilisababisha Mamlaka ya Mapato Tanzania kupata hasara ya shs. 9,269,066.38/-
Bw. ATHUMANI AHMADI SIMBA alikuwa mshtakiwa Namba 3 katika kesi hii kwa kosa la kushindwa kulipa kodi k/ f cha 83(a) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura ya 438 R.E 2019, ambaye aliingia makubaliano na Serikali akakiri kosa kisha kulipa kiasi cha shs. 9,269,066.38/-.
Washtakiwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 3 jela kwa kosa la kwanza na la pili kila mmoja au kulipa faini shs. 250,000/= kila mmoja kwa kila kosa.
Kwa kosa la 3, wamehukumiwa kifungo cha nje mwaka mmoja kila mmoja.
Kesi hii iliendeshwa na wakili Salum Bhoki wa TAKUKURU Lindi.