Mahakama ya Wilaya Kibondo, Kigoma tarehe 7 Juni, 2023 imemtia hatiani mshtakiwa Paul Simon Singi katika Shauri la Jinai Na.124/2023.
Shauri hilo lilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mh. Sarah Mcharo na mshitakiwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kisanda katika Kijiji cha Magarama alikuwa anakabiliwa na makosa mawili ambayo ni; kuomba rushwa k/f 15(1)(a) cha PCCA(RE 2022) na kughushi k/v 333,335 na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Sura 16 RE 2022).
Mshitakiwa alitenda makosa hayo tarehe 22/5/2023 kwa lengo la kuhalalisha umiliki wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 3 kwa mwananchi Fabiano Daudi katika eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika Halmashauri ya Wilaya Kibondo.
Mshitakiwa baada ya kupokea rushwa alitengeneza nyaraka ya kughushi ikionyesha mauziano yenye thamani ya Tsh.800,000/- kwa kutumia jina la Mwenyekiti wa Kitongoji aliyemaliza muda wake Bw. Josephat Gwimo.
Mshitakiwa alikiri makosa yote na Mahakama kumhukumu kwenda jela miaka 3 au kulipa faini ya Tshs 500,000/- kwa kosa la kwanza na kwenda jela miaka miwili na nusu au kulipa faini ya Tshs.250,000/-kwa kosa la pili. Mshitakiwa alishindwa kulipa faini na kupelekwa katika Gereza la Nyamisivi kutumikia kifungo.