Juni 16, 2023 katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, limefunguliwa Shauri la Jinai Namba 63/2023 dhidi ya
a) WILLIAM METHEW MAKUFWE (Aliyekuwa Afisa Utumishi na Afisa Uchaguzi Msaidizi wa Jimbo la Rungwe ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete),
b) CHRISTOPHER MSAFIRI NYAKI (Aliyekuwa Mweka Hazina wa H/W Rungwe) na
c) CHRISTOPHER DAVID MWAKANYAMALE (Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Inter-Business).
Washitakiwa hawa wanashitakiwa kwa makosa ya Kula Njama k/f 32, Ubadhilifu k/f cha 28 na Matumizi Mabaya ya Mamlaka k/f cha 31 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Makosa haya waliyafanya baada ya kutumia kwa matumizi yao binafsi kiasi cha shilingi 17,400,000/= kilichotengwa kwa ajili ya kutoa elimu kwa wasimamizi wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, 2015.
Mshitakiwa wa kwanza baada ya kusomewa shtaka hili alikana na Mahakama ilimwachia kwa dhamana.
Taratibu za kuwapata washitakiwa wa pili na wa tatu zinaendelea kufanyika.
Shauri litaendelea mahakamani kwa kusikiliza maelezo ya awali tarehe 3/7/2023.