Juni 13, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Tanga, Mbele ya Mheshimiwa Hakimu Suniva Joseph Mwajombe, imefunguliwa kesi ya Uhujumu Uchumi Nambari Ecc.07/2023, Jamhuri dhidi ya Omary Ally Salehe ambaye ni Afisa Vijana Katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, Amina Rajabu Mbwana ambaye ni Afisa Mtendaji Kata ya Nguvumali Jijini Tanga, Selebosi Mhina Musatafa ambaye ni Diwani wa Kata ya Nguvumali na pia Mstahiki Meya Mstaafu wa Jiji la Tanga, Pilly Salum Shomari ambaye ni Mweka Hazina wa Kikundi Hewa. Wengine ni Mwajuma Abdallah Mwaimu ambaye pia ni Mweka Hazina wa Kikundi Hewa kilichotumika kujipatia mkopo katika Halmashauri ya Jiji la Tanga kinyume na Sheria.
Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakamani kwa Kufanya makosa ya kughushi, wizi, Matumizi Mabaya ya Mamlaka na kuisababishia Mamlaka iliyoainishwa Hasara ya Sh 5,000,000/= kinyume na sheria, fedha ambazo zilitokana na tengo la 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa ajili Mikopo wa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mwaka wa Fedha 2018/2019.
Washtakiwa wote hawakukidhi vigezo vya dhamana na wamepelekwa rumande na kesi itaendelea tarehe 20/6/2023 kwa ajili usikilizwaji wa hoja za awali.