Shauri la Uhujumu Uchumi Namba 27/2023 limefunguliwa Juni 14, 2023, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu DSM mbele ya Mhe. Ngimilanga, ambapo Bw. Eliud Jones Kijalo, aliyekuwa Mhasibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Utalii, ameshtakiwa kwa makosa 206 ya Kughushi, Matumizi mabaya ya mamlaka, Ufujaji na Ubadhirifu, Utakatishaji wa fedha haramu na kuusababishia mfuko hasara ya shilingi bilioni 4.03.
Mshatakiwa hakujibu chochote kwakuwa Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na amepelekwa mahabusu hadi tarehe 28 Juni ambapo shauri litatajwa.
Shauri la Uhujumu Uchumi namba 26/2023 limefunguliwa tarehe 13 Juni, 2023 mbele ya Hakimu Mhe. Mrio wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo washtakiwa 8 ambao walikuwa waajiriwa wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), walisomewa mashtaka 48 ya kuendesha genge la uhalifu, kughushi, uchepushaji, kuwasilisha nyaraka za uongo na kuisababishia wakala hasara ya shilingi bilioni 2.16.
Washtakiwa hawakujibu chochote na shauri litatajwa tarehe 27 Juni, 2023
Juni 15, 2023, limefunguliwa shauri la Uhujumu Uchumi namba 29/2023 katika mahakama hiyo hiyo mbele ya Hakimu Mhe. Kabate ambapo Mshtakiwa Simon Masumbuko amesomewa mashtaka matatu ya kughushi, utakatishaji wa fedha haramu na kusababisha hasara ya shilingi bilioni 14, na Mshtakiwa amepelekwa mahabusu hadi tarehe 28 Juni, 2023, shauri hilo litakapotajwa.