Mahakama ya Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, mnamo Juni 6, 2023 katika Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 02/2023, mbele ya Hakimu Mkazi Mh. Lyon, Mshtakiwa amekiri makosa yake na mahakama imemtia hatiani.
Mshtakiwa huyo ni Bw. Ernest Mwambozi (Mwalimu Mkuu S/M Kamsamba) aliyeshitakiwa kwa kosa la Matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na k/f cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022.
Shtaka lingine ni kuisababishia hasara Serikali kinyume na Aya ya 10 (1) ya jedwali la kwanza na k/f 57(1) na 60 (2) ya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 marejeo ya 2022.
Baada ya Mahakama kuzingatia hoja za mshtakiwa za kuomba asipewe adhabu kali, Mahakama imeamuru Mshtakiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja.
Adhabu hiyo inaenda sambamba na kutakiwa kurejesha kwa mwajiri wake (H/W Momba), kiasi alichoiba sh. 1,080,000/= ambazo Mshtakiwa ameshazirejesha.