Mei 29, 2023, katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanga limefunguliwa Shauri la Uhujumu Uchumi namba 2/2023, ambapo washtakiwa ni 1. Zefrin K.Lubuva (aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji H/W Mwanga), 2.Mwajuma H.Muna (aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Mji Mdogo Mwanga) 3.Hassan A.Hassan (aliyekuwa Kaimu Mweka Hazina wa H/W Mwanga) na 4.Regnald P. Massawe (Kaimu Afisa Mtendaji Mamlaka ya Mji Mdogo Mwanga) kwa makosa ya matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri (washtakiwa wote) na matumizi mabaya ya mamlaka (mshtakiwa wa kwanza).
Washtakiwa hao walitenda makosa hayo na kusababisha mshtakiwa wa kwanza kulipwa posho za ‘extra duty’, ambazo hakustahili baada ya kuonesha kuwa ameshiriki kazi ya ukusanyaji wa mapato ya mchanga katika korongo la Libya Kisangiro, lililopo Mji Mdogo wa Mwanga katika vipindi tofauti tofauti.
Mshtakiwa wa kwanza hakufika Mahakamani licha ya kufikishiwa wito kupitia kwa mwajiri wake, hivyo washtakiwa wa pili hadi wa nne waliokuwepo mahakamani walisomewa makosa yao na kukana.
Washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kukidhi masharti.
Kesi hiyo imefunguliwa na Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Furahini Kibanga mbele ya Hakimu Mfawidhi Mhe. Mfanga.
Kesi imepangwa tena tarehe 20/06/2023 kwa ajli ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali na pia mshtakiwa wa kwanza amechukuliwa hati ya wito Mahakama ili ahudhurie siku hiyo.