Juni 01, 2023 imefunguliwa Kesi ya Uhujumu Uchumi namba ECO. 04/2023 katika Mahakama ya Wilaya ya Songwe, mbele ya Mh. Lugome.
Kesi hiyo ni Jamhuri dhidi ya Lington Mbuzi, Mkusanya Mapato katika H/W ya Songwe, Mkoani Songwe.
Hati ya Mashtaka imesomwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Conrad Kabutta kwamba kati ya tarehe 06.05.2017 na 10.10.2019, Mshtakiwa akiwa na nia ovu alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kupeleka fedha kwa Mhasibu wa H/W ya Songwe au kuweka kwenye akaunti ya H/W ya Songwe kiasi cha shilingi 13,913,488/= kinyume na Memoranda namba 37(2) na 50(5) ya Memoranda ya Fedha ya Serikali ya Mtaa ya mwaka 2009 kwa ajili ya kujipatia maslahi binafsi.
Pia mshtakiwa anakabiliwa na tuhuma nyingine ya Ufujaji na Ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa sura ya 329 marejeo ya mwaka 2019, ambapo mshtakiwa anadaiwa kati ya tarehe 06 Mei, 2017 na 10, Oktoba 2019 Lington Mbuzi akiwa Mkusanya mapato katika H/W ya Songwe Mkoani songwe alifanya ubadhirifu wa kiasi cha shilingi 13,913,488/= mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Songwe zilizofika kwenye himaya yake akiwa mtumishi wa umma.
Mshtakiwa amekana makosa yake na amepewa dhamana baada ya kukidhi masharti yote ya dhamana.