Mei 31, 2023 katika Mahakama ya Wilaya ya Songwe mbele ya Mhe. Lugome imefunguliwa Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. ECO 05/2023 Jamhuri dhidi ya Paschal Mushi – Mhasibu Halmashauri ya Wilaya ya Songwe.
Mshtakiwa akiwa na nia ovu kati ya 07.04.2020 na 24.05.2021 alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuweka fedha kwenye akaunti ya Halmashauri ya Wilaya Songwe kiasi cha sh. 14,470,135/= ndani ya muda uliotakiwa, kinyume na Memoranda ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 2009, kwa ajili ya kujipatia maslahi binafsi.
Mshtakiwa pia anakabiliwa na tuhuma ya ufujaji na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2019. Kwamba kati ya Aprili 7, 2020 na Mei 24, 2022 akiwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya Songwe alifanya ubadhirifu wa sh.14,470,135/= mali ya H/W Songwe.
Mshtakiwa amekana makosa yote na amepewa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana.
Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU katika shauri hili ni Conrad Kabutta.